Aliambiwa ananuka kama mbuzi, sasa awaonyesha yeye ni simba, tazama alivyofanya.......

Gavana Mvurya aungana na kina mama kucheza ngoma
ya kitamaduni katika mojawapo wa hafla katika kauti ya Kwale 
Imetolewa: www.standardmedia.co.ke
Gavana wa Kwale SalimMvurya ana sababu za kushangilia baada ya Kaunti ya Kwale kutajwa kama mojawapo wa kaunti ambazo zinatumia pesa za miradi ya maendeleo kwa njia sawasawa.
Taarifa katika gazeti la Nation zinasema Kaunti ya Kwale ilitumia asilimia 57.3 ya matumizi yake ya maendeleo, hiki kikiwa ndicho kiwango cha juu zaidi cha matumizi katika mwaka wa serikali ulioisha Juni 30.
Zamani, Mvurya alikuwa afisa wa maendeleo ya kijamii akifanya kazi na shirika la Plan International na huenda hapo ndipo alikereka na umaskini mkubwa ulioenea katika eneo la Kwale. Alipochaguliwa Mvurya aliyapatia kipaumbele maswala ya kuimarisha jamii kama vile kutengeneza  barabara, maji  na elimu na kutenga zaidi ya shilingi Milioni 400 kwa miradi hiyo.
 Taarifa hizo bila shaka huenda zikaweka kicheko cha ushindi katika midomo ya Mvurya na wafuasi wake hasa ikizingatiwa  kuwa amekuwa akipata upinzani mkali kutoka kwa baadhi ya wanasiasa katika kaunti ya Kwale na Mombasa kwa ujumla.
Ni hivi majuzi tu ambapo Gavana Mvurya alipoteza wadhifa wake kama naibu mwenyekiti wa baraza la magavana humu nchini, wadhifa uliochukuliwa na Gavana wa Taita Taveta Ben Mruttu.
Kutolewa kwa taarifa hizo huenda kukawatia aibu waliombandua mamlakani ya naibu mwenyekiti hasa kwa kuwa harakati zake za kuleta maendeleo katika kaunti ya Kwale zimeonyesha kuzaa matunda.
 Wanaomjua Mvurya wanasema kuwa hana ukabila, upendeleo na ubadhirifu wa fedha za umma. Pia anasemekana hapendi siasa za malumbano na hili lilifanya akakosa kuhudhuria vikao na wakuu wa chama cha ODM ambacho yeye ni mwanachama.
 Licha ya hivyo kuna wale wanaona kuwa hakuna alichoifanya kwa wakazi wa eneo la Kwale. Baadhi ya wabunge hasa wale wa kutoka Digo wakiwepo Suleiman Dori, Hassan Mwanyoha (Matuga) Zainab Chidzuga (Mwakilishi wa kina mama) Khatib Mwashetani (Lungalunga) na seneta Juma Boy hawamuungi mkono. Mbunge wa Gonzi Rai (Kinango) ndiye wake wa karibu.
Wengine ambao wanampinga na wanataka kuriithi wadhifa wa Gavana wa Kwale ni pamoja na aliyekuwa waziri  na mbunge wa Matuga ambaye sasa ni balozi wa Kenya nchini Tanzania Chirau Ali Mwakwere na spika wa kaunti ya Kwale Sammy Ruwa ambao kutokana na taarifa hizi za matumizi bora ya pesa za umma huenda wakawa na kibarua kigumu.
Mvurya anasema kuwa hana shida kubwa na wanasiasa wa Kwale wakimpinga kwa sababu ni haki yao kufanya hivyo. Kile kinachomkera zaidi ni kuingiliwa na wanasiasa wa Mombasa katika kutaka kumng’oa mamlakani.
 Yasemekana uhusiano kati yake na wanasiasa wa Mombasa ulianza kuingia ubaridi pale mbinu zake na zao zilipoanza kukinzana. Wakati ambapo wanasiasa wa Mombasa wanapenda siasa za mlengo wa kushoto zenye vitisho, makeke, malumbano na biashara, Mvurya ni mwanasiasa ambaye ni wa mlengo wa kati ambaye hapendi ubishi sana.
Fisi akitaka kumla mwanae husema ananuka kama mbuzi, na kwa sababu ya ubaridi huo Gavana Mvurya alidaiwa kuwa  na uhusiano wa karibu na wanasiasa wa mlengo wa Jubilee.
Gavana huyo hakushiriki katika kampeini za uchaguzi mdogo wa Malindi na hili halikuwafurahisha vigogo wa chama chake katika eneo la Pwani na hasa Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho ambaye pia ni naibu wa kiongozi wa chama cha ODM.
Mvurya pia alionekana kutounga mkono swala la maandamano ya kutaka makamishna wa tume ya uchaguzi nchini IEBC wabanduliwe na hili pia liliwakera zaidi viongozi katika chama hicho cha chungwa.
Kutokana na hayo viongozi hao walifanya bidii za mchwa kuhakikisha barabara ya Mvurya ya mwaka wa 2017 imetiwa mashimo ili kuhakikisha kufaulu kwake kumekatizwa.

Mwisho………




Comments

Popular posts from this blog

Safari ya Bamba Si Machero.......

What students did for their former Principal will leave you in tears.....

Who will save the poor of Central Province........